Pages

Friday, July 20, 2012

RISALA YA RAMADHANI YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN

RISALA YA RAMADHANI YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, KWA MWAKA 1433 HIJRIYA, 2012 MILADIA.


Ndugu Wananchi,

Assalam Aleykum Warahmatullah Wabarakatuh

Alhamdu Lillahi Rabil Alamin. Shukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa Viumbe vyote. Sala na Salam zimshukie Aliyetukuzwa na Muumba wetu, Mtukufu wa Daraja aliyeletwa kwa Rehema kwa ajili ya kuwaongoza waja wapate nusra ya Allah (Subhana Wataala).

Ramadhani tukufu imetufikia. Tuna wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu Azawajalla, kwa kutujaaliya umri tukaupokea Mwezi huu Mtukufu, Mwezi wa Ibada, Mwezi wa Furaha, Mwezi wa Neema. Kubwa zaidi ni kuwa huu ni Mwezi ambao kwa hekima zake Mola wetu ametuteremshia Quran, ambayo ndio “Uongofu kwa Watu” na yenye “hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi”. Aidha, ametutengezea usiku wa cheo kitukufu” usiku huo wa “Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu”.

Ndugu Wananchi,
Kutokana na neema hizi, sote tunawajibika Kwake kwa vitendo. Hivyo basi, madhumuni ya risala hii ni kuukaribisha Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani na kukumbushana baadhi ya mambo tunayostahiki kuyafanya katika Mwezi huu Mtukufu ili tufanikiwe hapa duniani na akhera twendako.

Wakati tunaukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, Mwenyezi Mungu ametupa mtihani wa maafa kwa kuzama meli ya MV SKAGIT iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kuja Zanzibar. Hadi jana usiku Watu wapatao 31 wamefariki, 123 hawajaonekana baada ya meli hiyo kuzama na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu watu 136 wameokolewa. Kuanzia asubuhi ya leo hadi mchana huu jumla ya maiti 22 zimepatikana. Katika kipindi hiki tumuombe Mola wetu atupe rehema zake, atughufirie makosa yetu na atujaalie subira.

Ndugu Wananchi,
Mwenyezi Mungu ametupa maelekezo kamili ya Mwezi huu Mtukufu katika Quran tukufu, surat Al-Baqara aya 183 hadi 187, aya ambazo Mashekhe na Maimamu wetu wamekuwa wakizielezea tangu Mwezi wa Shaaban na wanaendelea kutufundisha katika kipindi hichi na kutoa mawaidha yao.

Ndugu Wananchi,
Mafanikio ya wanadamu duniani yanakuwa makubwa kutokana na kuwa na mipango mizuri na madhubuti. Serikali zote duniani zinaendeshwa katika mtindo huo wa kujipanga na sisi hapa Zanzibar tunafanya hivyo hivyo. Mipango mbali mbali kama vile Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA), Dira 2020 na mengineyo ni miongoni mwa utaratibu huo. Lakini mipango tu haiwezi kutuletea mafanikio bila ya kuwepo mikakati ya utekelezaji, usimamizi mzuri na juhudi za utekelezaji. Wahenga walisema Mipango si matumizi”.

Jitihada mbali mbali zimekuwa zikifanywa na Serikali katika kuimarisha ustawi wa wananchi mmoja mmoja, vikundi na wananchi wote kwa jumla tukiwa na lengo kuu la kuwapunguzia wananchi wetu ukali wa maisha. Kwa mfano, Serikali imeamua kuwapunguzia gharama za Kilimo wakulima wetu na kuimarisha huduma hiyo ili kuwasaidia wananchi kuongeza kipato chao na kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje ya nchi. Kadhalika, hatua hii imelenga kupunguza tatizo la mfumko wa bei hasa kwa bidhaa za chakula.

Aidha, napenda kuwashukuru wakulima wetu kwa kujiandaa kuwapa huduma nzuri wananchi wetu hasa katika upatikanaji wa chakula kwa ajili ya futari. Naamini kuwa hisani, ukarimu na kuhurumiana vitazingatiwa katika biashara na utoaji wa huduma kwenye kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Serikali nayo itajitahidi kufanya kila linalowezekana ili kuwasaidia wananchi katika kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo yetu. Ni imani yangu kuwa kila mmoja wetu atatekeleza wajibu wake ili tuweze kutekeleza ibada zetu kwa wepesi huku nafsi zetu zikiwa zimeridhika. Tumuombe Mwenyezi Mungu atushushie baraka zote za Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.

Ndugu Wananchi,
Tumebahatika kuwa na kitabu cha Quran na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Pamoja na kuendesha ibada za Saumu, Sala na utoaji Sadaka katika mwezi huu, tutakuwa tumejipangia vyema ikiwa tutazidisha kusoma na Quran pamoja na Hadith za Mtume Muhammad, S.A.W. katika mwezi huu.

Kuporomoka kwa maadili ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili jamii yetu siku hizi. Sote tunaelewa madhara yake, yakiwemo maasi, uhalifu, kutotii sheria na hata kuanguka kwa kiwango cha elimu kwetu na kwa watoto wetu.

Tukirejea kwenye Quran na Hadith za Bwana Mtume S.A.W. tutajisaidia kupata ufumbuzi wa kuondosha madhara haya niliyoyagusia. Kwanza tukumbuke kuwa Quran Tukufu inanufaisha kila pahala na kila zama. Aya na sura za Quran zimejaa hekima (Ishara) ya elimu, sayansi, historia, maadili na kila fani. Kwa mfano, Aya ya 53 ya Surat FUS SWILAT, Juzuu ya 24, inatuambia “Tutawaonesha Ishara zetu katika upeo wa mbali katika nafsi zao wenyewe mpaka inabainika kwamba haya ni kweli. Je haikutosha kwamba Mola wako yeye ni Shahidi wa kila kitu?”

Kuhusu elimu katika mwezi kama huu iliteremshwa sura ya amri ya kusoma, aya ya kwanza ya Qurani, iliyosema:
“Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba binaadam kutoka tone la damu. Soma! Na Mola wako ni karimu kushinda wote. Ambaye, amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyekuwa hayajui!

Aya hizi zinatuhimiza wajibu wa elimu, zinatufundisha sayansi ya maumbile na zinatupa maarifa ya manufaa ya elimu na utamaduni, yakiwa ni funguo za maendeleo kwetu katika nyakati zote.

Ndugu Wananchi,
Elimu hii haipatikani bila ya kuitafuta. Tukumbuke kuwa Quran imeeleza katika Surat Ibrahim, Aya ya kwanza kuwa:

“Hiki ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu kwenye kiza uwapeleke kwenye mwangaza kwa idhini ya Mola wao, uwafikishe kwenye njia ya Mwenye Nguvu na Msifiwa”.

Ndugu Wananchi,
Nawasihi muutumie muda mwingi kuisoma na kupata maarifa ya Quran katika Mwezi huu, mafunzo ambayo yatadumu siku zote. Tukumbuke usemi wa Sayyidna Muhammad, Alayhi Salam kwamba:
“Asiyekuwa na chembe ya Quran moyoni mwake ni kama nyumba iliyobomoka”.
Imani zetu zitajengeka na maadili yetu mema yatarejea tutakapoisoma na kujifunza Quran na kuwa wakweli katika maisha yetu ya uongozi na ya kuongozwa. Uelewa wetu utayageuza maisha yetu katika njia sahihi. Baadhi ya wanazuoni wanasema “Elimu bila ya vitendo ni kama mti usiotoa matunda”. Hivyo tuazimie kuyatumia mafunzo ya Ramadhani katika maisha yetu yote ya kawaida kama ni matunda ya Saumu. Matunda ambayo ni muhimu kwetu.
Ndugu Wananchi,
Serikali yetu imo katika juhudi za kuwaandalia wananchi wake maisha bora, kwa kupitia mageuzi ya katiba na pia kwa kuhesabiwa watu, mambo yaliyomo katika sheria zetu. Quran na Hadithi za Bwana Mtume S.A.W zinatufundisha mshikamano, umoja na utiifu wa sheria. Ni vyema kufahamu na kuzingatia usafi wa nia (IKHLAS) ili tuwe watu wema na wenye kupenda amani na tusiokuwa na hasada au kupenda kutukuzwa.

Ndugu zangu nyote ni mashahidi ni mashahidi kuwa nchi yetu inaendelea kupata mafanikio. Uchumi wetu umeendelea kukua licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa. Wananchi na viongozi tumeshikamana kwa lengo moja la kuleta maendeleo ya haraka kwa nchi yetu. Nakunahini nyote tuendelee kushikamana, tuendelee kutii sheria na kujiepusha na vitendo vyote vya uvunjifu wa amani.

Tujikumbushe Surat Al – Imran, Aya 103 inayosema:
Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu; vile mlivyokuwa nyinyi kwa nyinyi maadui, naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu”.

Ndugu Wananchi,
Tuutukuze Mwezi huu wa Ramadhani kwa kukumbuka mafundisho hayo ya Quran na tuendeleze shughuli zetu za kimaisha katika hali ya amani, utulivu na mshikamano. Pamoja na hayo, tufanye biashara kwa misingi ya kutodhulumiana katika bei, viwango na vipimo.

Kuhusu hili la biashara, sote tunakubaliana kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni wa neema kibiashara. Lakini ni vyema kufanya neema hii iwe kwa wauzaji na kwa wanunuzi. Muuzaji anauza bidhaa zake nyingi zaidi, kwa hivyo anapaswa kuhakikisha zina ubora na anachuma faida kwa kiasi ya anachouza. Mnunuzi naye anahitaji kupewa bei iliyo nafuu, hasa kwa bidhaa ambayo Serikali imeipunguza kodi, kwani Serikali yenu kama kawaida itapunguza ushuru kwa bidhaa muhimu za chakula ili kuwawezesha wananchi kupata unafuu wa bei.

Wakati huo huo, ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa wanasafirisha bidhaa kama vile unga, sukari na mchele waliotozwa kodi ya chini na kuzisafirisha kwa njia ya magendo nje ya Zanzibar ili wapate faida kubwa. Kwa hakika jambo hili linasababisha upungufu wa baadhi ya vyakula na kuwasababishia shida wananchi wakati huu wa mwezi wa Ramadhan. Tunapaswa kuwa waadilifu katika hili na pia katika kuhakikisha vipimo vya kuuzia ni vya halali. Serikali imeweka mazingira mazuri ya biashara hasa katika Mwezi huu Mtukufu na ni wajibu wetu kuyatumia vyema ili tunufaike sote. Kama kawaida Serikali itakuwa macho kuona biashara inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kujali maslahi ya wananchi.

Natoa wito tuwe watendaji wema na ihsani baina yetu na hasa kwa masikini na wasiojiweza. Utoaji sadaka ni jambo la msingi na hatuna budi kulizingatia zaidi katika Mwezi huu, ili wenzetu wenye kipato cha chini nao mwezi huu wa Ramadhan uwe ni mwezi wa furaha kwao. Ramadhan Karim – basi tuwe na ukarimu kwa wenzetu na wageni wetu.

Aya 29-30 ya Surat Faatir inasema: “Hakika wale wanaosoma kitabu cha Mwenyezi Mungu na wakashika sala, na wakatoa kwa siri na kwa dhahiri katika tulivyowaruzuku, hao hutaraji biashara isiyobwaga; ili yeye amalize ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika yeye ni mwenye kusamehe, Mwenye shukurani”.
Nawasihi ndugu zetu wafanya biashara, wakulima, wavuvi na wahusika wote kuzingatia mambo hayo ili sote tuwe tumepata nafuu. Kutokana na hali nzuri ya hewa natumai tutakuwa na mwezi wa neema.

Ndugu Wananchi,
Kwa kuwa Ramadhani mwaka huu imetujia katika msimu wa Watalii na ziara za Wazanzibari wenzetu wanaoishi nchi za nje, tunapaswa kwa umoja wetu kuwaonesha wema wetu na mambo mema kwao. Tudumishe sifa yetu ya ustaarabu, uvumilivu na ustahamilivu, tushikamane nao na tuwaelimishe kwa upole kwa yale wasiyoyajua ya mila zetu. Tudumishe amani na tuhakikishe usalama kwa watu wote, hasa nyakati za usiku ambapo watu wengi wanakwenda misikitini kufanya ibada za Mwezi wa Ramadhan.

Sote kwa pamoja tujitahidi kuweka mitaa yetu katika hali ya usafi na Mamlaka zinazohusika na usafi ziongeze bidii kusafisha maeneo ya makazi na matembezi ya watu.

Tujitahidi kuzingatia mafundisho ya dini katika kupata ukamilifu wa saumu zetu. Wananchi wengine wasiowajibika na saumu kama kawaida watoe ushirikiano na wawe wastahamilivu kwa wenzao wanaofunga. Wale wasiowajibika kufunga kwa sababu mbali mbali wajitahidi kutumia fursa hii vyema bila ya kuwakirihisha wengine. Kwa upande wa madereva na watumiaji wote wa barabara tuzingatie usalama barabarani hasa wakati wa jioni ambapo watu wengi huwa wanakimbilia kuftari.
Jeshi letu la Polisi litaendelea kuimarisha ulinzi wa watu na mali zao kwa kushirikiana na vijana wa ulinzi shirikishi ili wananchi wapate utulivu na watekeleze saumu kwa amani. Ni wajibu tushirikiane na Jeshi letu la Polisi katika kulifanikisha suala hili.
Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia, napenda kugusia mambo mawili. Kwanza ni kwa wazazi na walezi kuzisimamia zaidi nyenendo za watoto wao katika Mwezi huu na kuwahimiza zaidi katika ibada na darsa. Pili, kwa vile tunakabiliwa na msimu wa Hijja, basi ni vyema kwa wanaofanya safari za Hijja kuwa na ushirikiano wa karibu ambao utaleta manufaa kwa wenye kukusudia kutekeleza ibada ya Hajji na Umra. Mwenyezi Mungu awape taufik wote na awafikishe kutimiza azma zao na kuwarejesha nyumbani kwa salama.
Namuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kutekeleza ibada za Saumu na nyenginezo katika hali ya umoja, mshikamano, amani na utulivu. Atuongezee mapenzi baina yetu ili tuzidi kuhurumiana. Atufanyie wepesi katika kupata riziki za halali na kumshukuru Mola wetu. Tunamuomba Mola wetu atuzidishie imani zetu kwake na tuwe wenye kujali maslahi ya wenzetu na tuwe watu wa kufanya ihsani ili tupate mavuno ya mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.
R A M A D H A N K A R I M
Assalam Aleykum Warahmatullah Wabarakatuh
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Popular Posts