Pages

Wednesday, July 18, 2012

UPOTOSHAJI WA ZIARA ZA CCM MIKOANI

Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa akizungumza na waandishi wa habari leo
YAH; UPOTOSHAJI WA ZIARA ZA CHAMA MIKOANI

Toka tarehe 03/05/2012 nimekuwa na ziara kadhaa za kichama katika mikoa mbalimbali kwa lengo la kukiimarisha Chama. Baadhi ya mikoa niliyofanikiwa kufika ni pamoja na Ruvuma, Njombe, Iringa,Mbeya,Kagera,Rukwa na Katavi. Ziara hizi zimekuwa zikilenga kufanya yafuatayo kati ya mengi niliyofanya:

1. Kukagua uhai wa Chama
2. Kukagua maendeleo ya uchaguzi ndani ya Chama
3. Kukagua miradi mbalimbali ya kiuchumi ya Chama
4. Kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM

Kwa muda sasa pamekuwa na juhudi za makusudi za kupotosha nia na madhumuni ya ziara hizi na kujaribu kuonyesha kuwa kinachofanyika hakina baraka za Chama na hivyo kimesababisha mgogoro ndani ya Chama, hasa kati yangu na Katibu Mkuu.

Juhudi hizi zimelenga kukatisha tamaa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Chama za kuwa karibu na wanachama wake na wananchi. Kwa bahati nzuri vyombo vya habari vinavyotumika kusambaza uzushi na uongo huu vinajulikana ni vya nani, hivyo ni rahisi kujua kwanini wanafanya wayafanyayo.

Kwa mfano, wanadai kuna pesa nyingi ninapewa mimi kama Katibu wa Itikadi na Uenezi na ninapewa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM bila Baraka za Katibu Mkuu wangu ambaye ndiye msimamizi wangu mkuu na kwamba hilo limezua malalamiko na migongano kati yetu.

Huu ni uzushi wa kitoto sana, kwani wanataka kuwaaminisha wana CCM na wananchi kwa ujumla kuwa mambo si shwari ndani ya CCM. Huku wakipuuza ukweli kuwa Katibu Mkuu wa CCM ndo msimamizi wa mapato na matumizi yote ya CCM, hivyo kama kuna ziara au jambo linalohusu matumizi ya pesa ndani ya Chama, lazima liwe na baraka zake.

Lakini wanafumba macho ili wasione kuwa, Katibu Mkuu wa CCM ndio mwenyekiti wa sekretarite ya Chama Taifa, hivyo sisi wajumbe wote wa sekretarieti tunafanya kazi chini ya maagizo na usimamizi wake wa karibu. Kama kuna mafanikio yeyote basi mwasisi wa mafanikio hayo ni Katibu Mkuu wa CCM Taifa ndugu Wilson Mukama, kwani yeye ndiye kiongozi wa sekretarieti hii.

Itakumbukwa kuwa nilipoanza ziara hizi, wapotoshaji hawa walituhumu ziara zangu kuwa zinalengo la kutisha baadhi ya watu wasigombee nafasi mbalimbali ndani ya Chama kisa wao na mimi tuna mitazamo tofauti ndani ya chama. Nilipowataka kulithibitisha hilo na wakashindwa, sasa wamekuja na tuhuma mpya.

Nawaomba wana CCM, wapenzi na mashabiki wa CCM na wananchi kwa ujumla kuupuuza uongo na uzushi huu kwani hauna ukweli wowote. Umetungwa na watu wenye roho mbaya wasioitakia mema CCM, wanaotamani kuona CCM haitulii na hivyo mambo yasimame ndio furaha yao. Sasa wakiona mambo yanakwenda viroho vyao vinawauma.

Nataka niwathibitishie sekretarieti ya Taifa ya CCM iko imara, thabiti, madhubuti na yenye mshikamano tukifanya kazi kwa pamoja na upendo chini ya uongozi imara wa Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Mukama.Wanao yatunga na kuyasambaza haya wanapoteza muda wao.

Nawathibitishia uzushi huu hauta athiri kasi yetu ya kujenga Chama chetu wala ari yangu binafsi katika kukitumikia Chama changu kwa nguvu zote. Hivi ninavyoongea tayari maandalizi yamekamilika ya mkutano mkubwa wa hadhara mjini Kigoma siku ya kesho tarehe 19/07/2012 kwa lengo la kuzungumza na wana Kigoma juu ya mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoukabili mkoa wa Kigoma.

Katika mikutano hii mingi nina ambatana na baadhi ya mawaziri wa wizara mbalimbali zenye maeneo ya utekelezaji kwenye mikoa husika. Kwa mfano Kigoma tutazungumzia hatua iliyofikiwa katika sekta ya Uchukuzi kwa maana ya reli, bandari na anga. Lakini mkoa huu una kero kubwa ya maji hasa mjini Kigoma. Kuna changamoto kadhaa kwenye serikali za mitaa, kuna mengi yanayoendelea ya ujenzi wa miundimbinu kama barabara nk.

Staili hii tunayotumia kwenye mikutano mingi ya hadhara ambayo kwakweli inatutofautisha sisi Chama tawala na vyama vingine vya saisa nchini, tuliizindua pale jangwani kwenye ule mkutano mkubwa wa kihistoria mwezi Mei mwaka huu! Staili hii imepewa jina la AHADI NI DENI. Hivyo wana Kigoma na maeneo mengine kaeni mkao wa kula, AHADI NI DENI inakuja kwenu.

Itakumbukwa tuliwaahidi katika mkutano wa Jangwani kuwa tutazunguka nchi nzima, lakini tofauti na wenzetu wanaotukana na kukashifu kila kinachofanyika na kilichofanyika sisi tunakwenda kupeleka majawabu ya changamoto mbalimbali kwenye maeneo yao. Na hii ndio tofauti ya vyama vya upinzani na Chama tawala. Wakati wao wanabeba matusi na kejeli kwenye mikutano yao, sisi tunabeba majawabu namtumaini kwa wananchi. Kwahiyo “ahadi ni deni” imelenga kuzipitia ahadi zetu kwa wananchi na namna spidi ya utekelezaji wake ilivyo.

Nawataka sasa, hawa wanaozusha maneno na kujaribu kupotosha ziara nizifanyazo mikoani kuacha mara moja, kwani kukaa kwangu kimya haina maana kuwa siwafahamu. Nawaonya wakiendelea nitawasema hadharani bila kumumunya maneno. Nasema inatosha, upotoshaji mliofanya unatosha, sasa basi.



KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI


Imetolewa na;



Nape Mose Nnauye
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
Itikadi na Uenezi

Popular Posts